Viongozi wa Jumuiya mbili za
Kiislam Kisiwani Zanzibar wanaotuhumiwa kwa makosa tofauti ya kutoa
lugha za uchochezi na kusababisha ghasia na vitendo vya uvunjifu wa
amani uliopelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara ambao leo
walifikishwa Mahakama Kuu ya Vuga mjini Zanzibar, wamerudishwa tena
Rumande.
Kesi hiyo ambayo inawakabili
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikhe Faridi Hadi Ahmedi na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe Mselem Ali Mselem, Mussa Juma
Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman,
Hassan Bakar Suleiman na Ghalib Ahmada Omar iliitwa mahakama kuu kwa
kutajwa baada ya kuahirishwa mwezi uliopita.
Hata hivyo, kabla ya kutajwa tena
kwa kesi hiyo, huku kukiwa na ulinzi mkali wa Makachero wa Polisi na
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, ndani ya Mahakama hiyo kulizuka
mabishano makali ya kisheria huku kila upande ukionyesha ujuzi wao wa
kisheria.
Kwa upande wa Mawakili wa
Watuhumiwa Bw. Salum Toufik na Bw. Abdallah Juma Kaka, wakiwasilisha
hoja mbalimbali za uvunjifu wa haki za watuhumiwa ikiwemo ya kunyolewa
ndevu wakiwa Rumande katika Chuo cha Mafunzo jambo ambalo ni kinyume na
uhuru wa kuabudu kwani wamesema ndevu kwa mashehe ni sehemu ya ibada.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo,
Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ramadhani Nassibu,
akinukuu vifungu vya sheria vilivyopo kwenye Katiba ya Zanzibar na
kusema kuwa kama kuna haki zinazovunjwa na chombo chochote ama mtumishi
wa Serikali kuna mahala pengine pa kupeleka malalamiko hayo.
Baada ya mabishano hayo, Mrajisi
wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru watuhumiwa wote
warudishwe tena rumande hadi Novemba 20, mwaka huu itakapokuja tena
katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kutajwa.
No comments:
Post a Comment