Uchaguzi huo uliokuwa ukitafuta wawakilishi wa nafasi mbalimbali za Umoja wa Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam na kusimamiwa na Mbunge wa Ilala, Musa Zungu, ulilazimika kurudiwa baada ya wagombea wawili kupata alama sawa.
Kabla ya kurudi katika ukumbi wa uchaguzi majira ya saa 9:10, vurugu zilianza kujitokeza ambapo wapambe wa mgombea Salim Salim ‘Chicago’ walikuwa wakihaha kuhakikisha anaibuka kidedea.
Hata hivyo mpambe wa mgombea mwingine, Nicolaus Msemo, alikuwa makini na kumfuata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Idd Toatoa na kuanza kupigana naye kabla ya kuamuliwa na wanachama waliokuwa karibu yao.
Nafasi ya uwakilishi wa Baraza Kuu mkutano mkuu Taifa kupitia Jumuiya ya Wazazi mkoa huo ilikuwa ikiwaniwa na wagombea wanne ambao ni Salim Chicago, Msemo, Mohmed Honelo na Tambwe Hizza.
Honelo na Tambwe walienguliwa mapema kutokana na kura zao kuwa chache huku wagombea hao wawili wakirudi katika uchaguzi.
Aidha, nafasi ya uenyekiti Umoja wa Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam ikichukuliwa na Mbunge wa Afrika Mashariki, Angela Kiziga aliyeibuka kidedea kwa kura 170.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) CCM mkoani Dar es Salaam, Zarina Madabida, aliyekuwa akitetea kiti chake, ameanguka na nafasi yake kuchukuliwa na Janeth Masaburi, Mke wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
No comments:
Post a Comment