Treni ya reli ya kati ambayo imeanza kazi ya kusafirisha abiria mjini Dar es Salaam
USAFIRI wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza leo. Treni
ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati
ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC)
imetumia wastani wa dakika 30 kufika katikati ya jiji.
Treni ilioanza kazi leo
iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini) moja ikiwa imefungwa nyuma
na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria
wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba
wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu huku wanafunzi wakitakiwa
kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.
Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo ambao ni
wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi
Kitengo cha Reli. Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni
hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es
Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni,
ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini.
Alisema jumla ya mabehewa ya treni
14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini,
ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya kusafirisha abiria kuingia
na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine ikienda.
Akifafanua zaidi alisema
kitendo cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini
kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia
sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali ingelazimika kukodi injini
gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku.
Hata hivyoDk. Mwakyembe
amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa upungufu
utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya
marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. Mwandishi
wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo.
Awali akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni
hiyo itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu
na itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa
9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa
nne usiku.
Uchunguzi uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la treni
linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango minne,
feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa
abiria ambao watakuwa wamesimama.
Aidha mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha. Treni
ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la
Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo
Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji).
|
No comments:
Post a Comment