Na:waandishi wetu.
.
Lahusishwa na
uchomwaji makanisa
·
Uamsho walibebeshwa
mzigo usio wao
·
Dai la vitambulisho
bandarini Dar laleta hofu mpya
“Kama
hoja ya kudai kiti cha Zanzibar katika Umoja wa mataifa ingetolewa na katibu
kata au mjumbe wa nyumba kumi, ingekuwa huru na kutazama yenyewe kama ilivyo,
lakini kwa kutolewa hadharani na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad, hoja hiyo inafichua mambo makubwa na kujenga dhana kuwa,
hata kundi la Uamsho wa Mihadhara ya Kiislamu la Zanzibar, lililoibua vugu vugu
hilo na kuishia kwenye uchomwaji moto wa makanisa lilibeba ujumbe usio wao.”
Hayo
ni maelezo ya mmoja wa wachangiaji wa mjadala mzito ulioibuliwa wiki iliyopitan
na Maalim Seif, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), chenye
kuunda Serikali Mseto na CCM huko Zanzibar.
Katika
kauli yake hiyo, Maalim Seif, alisema kuna haja kwa Zanzibar kurejeshewa
kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).
Alitoa
kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Wilaya na Majimbo wa Chama cha
Wananchi (CUF), katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, kisiwani Pemba wiki iliyopita.
Kiongozi
huyo wa pili katika Serikali ya mseto alisema kuwa, Zanzibar kabla ya Muungano,
ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti chake UN, hivyo ni wakati sasa kurejeshewa
mamlaka kamili, ili iweze kutambulika tena kimataifa.
Maalim
Seif, alisema; hoja kubwa ambayo Wazanzibari wanatakiwa kujadili katika
mchakato wa maoni ya Katiba mpya ni muundo na mfumo wa Muungano.
“Zanzibar
tunayo Katiba yetu ya mwaka 1984, ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya
Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa ni la
Muungano na hili haliwezi kuepukwa,” alisema Maalim Seif.
Maalim
Seif, aliwataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao, kwanza katika mchakato
wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba na kuacha tabia ya kutetea misimamo
ya vyama badala ya maslahi ya nchi na wananchi wake.
Kisha
akaongeza: “Katiba ya nchi ni mali ya wananchi, siyo ya chama chochote, lakini
najua kila chama kina katiba yake na hiyo ndiyo itabakia kuwa katiba na
mwongozo wa chama husika, kwa hivyo! ndugu zangu naomba tulifahamu hili na
tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza,” alisema Maalim na kupigiwa makofi na
wanachama.
“Mimi
najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na muungano wa
mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumue…Yote hayo ni maoni na kila
mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu
ukifika nendeni mkatoe maoni hayo kwa uwazi,” alisema Maalim Seif.
“Wakati
wenu ukifika nendeni mkatoe maoni yenu kwa uwazi bila ya hofu hiyo ni haki yenu
ya kikatiba,” aliongeza.
Kauli
ya Maalim Seif inapingana na ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya
maoni ya katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, ambaye alizitaka taasisi, vyama na
makundi mengine kutowapandikizia wananchi maoni badala yake wawaache watoe
maoni yao.
Kwa
muda mrefu sasa kumekuwa na madai kadhaa mitaani kuwa, Chama cha Wananchi CUF,
kinatumia dhana ya udini kujieneza. Ingawa chenyewe kimekuwa kikikana madai
hayo lakini bado dhana hiyo haijafutika katika mawazo ya watu.
Lakini
jambo linalotia shaka ni uwiano wa wazi wa hoja baina
Maalim Seifu na zile za kundi la uamsho, ambalo mapema mwaka huu,
liliibua maandamano na ghasia zilizpeleka kuchomwa moto baadhi ya makanisa,
likiwepo la Katoliki na Tanzania Assemblies of God.
Wanauamsho
katika ujumbe wao wa maelezo na mabango walidai kuwa Zanzibar, imekuwa
ikinyonywa, hivyo inahitaji kuwa huru itambulike kimataifa.
Aidha
kundi hilo lilipinga zoezi la kukusanywa kwa maoni ya kuandikwa kwa katiba mpya
mpaka kwanza Wazanzibar wapewe nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu aina ya
Muunganao wanaoutaka. Dai hili linafanana sana na hoja ya Maalim Seif.
Baadhi
ya waliojadili suala hilo kwenye mitandao ya kijamii, wiki hii, wametofautiana
na Wazanzibar wengi wakimuunga mkono kiongozi huyo wa Serikali ya mseto, lakini
Wabara wengi wakipingana naye.
Miongoni
mwa waliotoa maoni yao ni, Bw. Haji Ismael wa Pemba, ambaye aliliambia jibu la
Maisha kuwa, hoja aliyonayo Maalim Seif, ni ya Wapemba wote na kwa kweli
wangependa kuachana na Muungano, ili wampendeze mola wao.
“Hoja
hii nakuambia wala sio ya Uamsho, wale ni mashujaa walioibeba lakini hii ni
hoja ya Wazanzibari wote. Kwa kweli kuna tofauti kubwa sana baina ya Wabara na
Wazanzibar, Wabara wengi wanaishi maisha ya mseto, wakati Wazanzibar wanaishi
maisha ya ki-Islamu. Mwezi mtukufu, Zanzibar huwezi kuona uchafu unafanyika,
lakini Bara sio hivyo wanaweza kukaanga nguruwe uwanjani wakala na kujilamba,
hivyo ni bora muungano utazamwe upya ili utoe nafsi kwa Waislamu kutekeleza
nguzo zao zote za uislamu.” alisema Bw. Haji.
Ingawa
Maalim Seif, hakufafanua kauli yake ya Zanzibar kuwa na kiti chake katika UN,
lakini anamaanisha kwamba Zanzibar inapaswa kuwa na mamlaka yake kamili.
Kwa
maana hiyo ikiwa Zanzibar itarejeshewa kiti chake katika UN, hapatakuwepo na
Muungano tena kwa kuwa itakuwa ni nchi kamili ambayo inatambuliwa na UN na Jumuiya
ya kimataifa kwa ujumla.
Tangu
Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kuanza kazi hiyo, kumeibuka kikundi
kinachofanya kampeni misikitini (Uamsho), kutaka Zanzibar kujitenga katika
Muungano huku wengine wakitetea kuwepo kwa Muungano wa mkataba.
Vile
vile, baadhi ya Wazanzibari wakiwemo mawaziri na makada wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wamesema kuwa, kuna haja ya kuwa na Muungano wa mkataba kwa lengo la
kumaliza kero zinazolalamikiwa.
Miongoni
mwa makada wa CCM waliotaka Muungano wa mkataba ni Waziri asiye na Wizara
Maalum, Mansour Yusuf Himid, na mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Ali
Nassoro Moyo.
Hata
hivyo, baadhi ya makada wamewashambulia na kuwatisha wanachama wa chama hicho
wanaotoa maoni tofauti na sera ya CCM ambayo ni muundo na mfumo wa serikali
mbili.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wiki iliyopita wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa Jimbo lake la Kitope, alisema; wanaopingana na sera
ya CCM kuhusu muungano warejeshe kadi zao za uanachama, badala ya kusubiri
kufukuzwa.
Naye
Mbunge wa Uzini (CCM), Dk. Mohammed Seif Khatib, Alhamisi iliyopita akizungumza
na waaandishi wa habari mjini Dodoma akiwa na wabunge zaidi ya 30 kutoka
Zanzibar alieleza kushangazwa na wanachama wanaotoa maoni ya kuvunja Muungano.
Khatib
ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wa CCM Zanzibar, alisema chama hicho kinapaswa
kuwachukulia hatua kwa maelezo kuwa walipata nyadhifa zao kwa kutumia ilani ya
CCM inayoeleza wazi kuwa sera yake ni ya Muungano wa serikali mbili.
Hadi tunaenda mitamboni juhudi za kumpata
msemaji wa CUF, kueleza ikiwa kuvunja muungano ndio msimamo wa chama hicho
hazikufanikiwa lakini hata hivyo bado zinaendelea.
Wakati huo huo, utaratibu
mpya wa safari za Zanzibar, kupitia boti katika bahari ya Hindi, wa kuwataka
wasafiri kuonesha vitambulisho vyao kabla ya kukatiwa tiketi umelalamikiwa na wasafiri wengi kuwa ni wa
kustaajabisha na haukutangazwa.
Uchunguzi wa gazeti hili
umebaini kuwa huo ni utaratibu
uliokuwepo huko nyuma ingawa ulikuwa haufuatiliwi hadi zilipotokea ajali mbili
za majini na kuuaa watu wengi, ndipo mamlaka ya usafiri wa majini na nchi kavu
SUMATRA walipotangaza amri ya kusimamiwa.
Baadhi ya wasafiri
wameonesha wasi wasi wao kuwa, huenda kuna jambo nyuma ya pazia kwamba, kuwa
wanaopanda boti kuja bara hawaulizwi vitambulisho, lakini wakirejea wanatakiwa
kuwa navyo.
No comments:
Post a Comment